KISWAHILI KIDATO CH KWANZA MAADA ZOTE



SOMO LA: KISWAHILI
KIDATO:CHA KWANZA
MADA YA  KWANZA: MAWASILIANO
Katika mada hii unatarajiwa kuelewa fasili ya mawasiliano na jinsi mchakato wa mawasiliano unavyofanyika. Utaelewa dhana ya lugha na vipengele muhimu vinavyokamilisha fasili ya lugha. Utaelewa dhima kuu za lugha, matumizi na umuhimu wake. Vilevile katika mada hii utajifunza juu ya lafudhi na matamshi mbalimbali ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili.

Lugha kama Chombo cha Mawasiliano
Mawasiliano ni mchakato wa kuhawilisha taarifa kwa njia ya ubadilishanaji wa mawazo, hisia, malengo, tabia, matarajio, mitazamo kupitia mazungumzo, ishara na maandishi. Ni ubadilishanaji wa taarifa unaoleta maana baina ya pande mbili au zaidi ambazo zinaweza kuwa viumbe hai au kinyume chake. Sasa hapa sisi tutajikita katika mawasiliano yanayofanywa baina ya viumbe wanaotumia lugha (ambao kimsingi ni binadamu).

Maana ya Mawasiliano
Lugha ni nyenzo muhimu sana katika mawasiliano ya binadamu. Ulishawahi kujiuliza kwamba mwasiliano yangekuwaje pasipokuwepo lugha?Mwalimu angekua anatumia mtindo gani kukufundisha darasani au wewe ungemwombaje kalamu rafiki yako? (Unasema ungewasiliana kama wanavyowsiliana watu wasiosikia au kuzungumza?) Hao pia wanawasiliana hivyo kwa sababu wana maarifa ya lugha.
Mafumbuzi ya kisayansi na teknolojia, yote haya yasingewezekana pasipo kutumia lugha, usingeweza kusogoa (kuchat) na marafiki zako kwenye facebook, usingeweza kumwandikia ujumbe rafiki yako kupitia simu yako na kadhalika.
Umeona sasa jinsi lugha ilivyo muhimu katika mwasiliano?Kabla hatujaona umuhimu huu hebu tuangalie fasili/maana ya lugha.
Kuna mitazamo mbalimbali juu ya fasili ya lugha lakini kwa ujumla lugha inaweza kufasiliwa kama mfumo wa sauti za nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano yao ya kila siku ili kuelezea hisia, mawazo, matakwa na mahitaji yao.
Kulingana na fasili hii tunaweza kubainisha maneno ya msingi yanayojitokeza katika fasili ya lugha, maneno hayo ni pamoja na haya yafuatayo:

Lugha ni mfumo
Kila lugha ya mwanadamu imeundwa katika mifumo miwili mikuu; mfumo wa sauti na mfumo wa maana. Lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya neno, maneno nayo huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai, vishazi, sentensi na aya. Mfano; k+u+k+u – kuku
Mtoto + anatembea – mtoto anatembea
Katika muunganiko huu wa maneno na miundo mbali mbali, huwa kuna kanuni na sheria zinazodhibiti mfuatano wa kila kipashio. Kuna kanuni zinazodhibiti mfuatano wa sauti, mfuatano wa mofimu, mfuatano wa maneno na hata mfuatano wa sentensi. Kwa maana hiyo, lugha ya mwanadamu ni mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu maalumu ambazo zikikiukwa basi kunakuwa hakuna utimilifu wa lugha husika. Sheria hizi zinazotawala mpangilio wa viunzi vya lugha hiyo ndizo zinazowawezesha watumiaji wa lugha fulani kuelewana.

Lugha ni mfumo wa sauti nasibu
Lugha ni ya nasibu kwa maana kwamba, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno (kwa mfano jiwe) na kitu chenyewe tunachotumia katika ujenzi na matumizi mengine (maana na kirejelewa). Hii ina maana kwamba, maumbo ya ishara za kiisimu hayana uhusiano wowote au mfanano wowote na maana ambazo tunayapa. Kwa mfano neno “jiwe” hakuna watu waliokaa na kusema kuanzia leo hili litaitwa jiwe. Vile vile hakuna uhusiano wowote kati ya neno “jiwe” na umbo linalorejelewa. Uhusiano wake ni wa nasibu tu na hutofautiana kutokana na lugha moja na nyingine. Jiwe mnaliitaje katika lugha yenu? Basi huo ndio unasibu wa lugha.

Lugha ni maalumu kwa mwanadamu
Lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho amejaliwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe mwingine ambaye si binadamu mwenye uwezo wa kuzungumza na kutumia lugha. Hii ina maana kuwa kuna sifa fulani za lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule isipokuwa mwanadamu. Ingawa ndege, mbwa, nyuki, tumbili wanaweza kuwasiliana, mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa yanadhibitiwa na hisia tu kama hofu, njaa, na ishara za kutoa taarifa. Binadamu ana uwezo wa kujifunza lugha mbalimbali na kuitumia katika mazingira yake na kitu ambacho wanyama hawawezi. Kwa mfano, ukimchukua paka wa china na kumleta Tanzania atatoa sauti ile ile sawa na paka wa Tanzania kwa kueleza shida ile ile au kutoa ishara ile ile.

Lugha ni mfumo wa ishara
Uishara wa lugha unamaanisha kuwa maneno huambatanishwa/huhusishwa na vitu, matendo,mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu. Vile vile, yale tunayoyasoma katika maandishi ni ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika muktadha wa mawasiliano. Hivyo basi, tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo wa alama za lugha hiyo na kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu vinavyowakilishwa.

Lugha hutumia sauti
Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti ambazo hutengenezwa na ala za sauti. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba:
  1. Mtoto hujifunza kuzungumza kabla hajajifunza kusoma na kuandika.
  2. Mtoto hujifunza lugha moja kwa moja bila kufikiri kadiri anavyokuwa
  3. Maandishi yalikuja baada ya mazungumzo
  4. Maandishi huwasilisha yale yanayozungumzwa
  5. Watu kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza kuliko kuandika
Kuna mambo mengi ya muhimu katika sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vema kwa kutumia maandishi. Mambo hayo ni kama, kiimbo, toni, mkazo, kidatu; haya ni muhimu katika mawasiliano lakini hayawezi kuwasilishwa kisawasawa kwa kutumia maandishi

Lugha ni kwa ajili ya mawasiliano
Kwa kutumia lugha binadamu anaweza kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi kuvifanya.Vile vile lugha hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio yetu, kucheza, kufanya kazi n.k. Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha ambayo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano.

Mfumo wa Lugha
Hoja kuwa lugha ni mfumo inamaanisha kuwa lugha ina muundo unaohusisha viambajengo mbalimbali. Viambajengo au vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa pamoja, vipashio hivi hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo hazina maana au kama haziwasilishi ujumbe wowote basi tunasema haziwi lugha.
Dhima za Lugha katika Mawasiliano
Fafanua dhima za lugha katika mawasiliano
Baadhi ya dhima za lugha ni pamoja na hizi zifuatazo:
  1. Ujumi: ujumi ni hali ya kutumia maneno ya lugha fulani kwa ufundi na ustadi wa hali ya juu kwa lengo la kuburudisha na kuwavutia watu wengine. Baadhi ya watu hutumia lugha kwa dhima hiyo, ili maksudi wasomaji au wasikilizaji wao wavutike na kuburudishwa na Lugha hiyo. Maeneo yatumikamo lugha yenye ujumi wa kiwango cha juu ni kwenye matangazo na kwenye fani ya utunzi wa mashairi.
  2. Utambuzi: Ni hali ya kufikiria kwa makini, kukokotoa na kutoa majibu ya maswali tofauti ndani ya ubongo. Chombo kikuu kitumikacho kutoa majibu hayo ni lugha. Kutokana na muktadha huo tunaweza kusema kwamba lugha hutumika kama chombo cha utambuzi.
  3. Hisia: ni fikra za ndani alizokuwa nazo kiumbe mwanaadamu. Tunapotaka kuonyesha hisia zetu na vilevile kuwavuta wengine kwa maneno mazito yanayoweza kumtoa msikilizaji machozi ya huzuni au ya furaha tunachagua maneno makali yenye hisia.
  4. Kujielezea: Hali ya mtu kudhihirisha mambo mbalimbali aliyokuwa nayo ndani ya moyo wake. Kwa mfano mtu anaposema nina furaha sana. Hapa mtu anatowa msisitizo wa kuonyesha kiwango cha furaha alichonacho, hili linafanyika kwa kutumia lugha. kwa ufupi tunachoweza kusema hapa ni kwamba lugha hutumika kwa ajili ya kujielezea.
  5. Kuamuru: Ni kutoa maelekezo kwa njia ya kuamrisha. Kwa mfano hakimu anamuhukumu mshitakiwa kwakumuamuru ‘Ninakufunga miaka mitatujela’. Hapa lugha inatenda kazi ya kuamuru.
  6. Kushirikiana: ni hali ya kutenda kitu kwa pamoja au hali ya kuwa na ubiya kwenye jambo. Lugha huwezesha watu kujenga mahusiano ya siri baina ya watu wawili au zaidi na kuweza kujitengenezea njia zao za kuwasiliana pasipo wengine kuelewa.
  7. Kuonesha: kumuelekeza mtu kitu kwa njia ya kuashiria. Unapotaka kuonesha jambo ni lazima utumiye lugha kwa njia moja au nyengine.
Matumizi na Umuhimu wa Lugha
Lugha hutumika kama chombo, zana, kifaa au njia ya kufikia lengo fulani. Baadhi ya matumizi ya lugha ni pamoja na haya yafuatayo:
  1. Kuwasiliana:- Lugha hutumika kupashana habari
  2. Kuunganisha- Lugha hupatanisha na kuleta uelewano miongoni mwa wanajamii. pia lugha huweza kutofautisha jamii moja na nyengine.
  3. Kujenga jamii- lugha huleta/huhimiza shughuli za maendeleo ya jamii, huleta amani na mshikamano katika jamii.
  4. Kufundishia- Lugha hutumika katika kufundishia elimu.
  5. Kutambulisha- Lugha hutumika kutambulisha jamii ya watu fulani.
  6. Kuhifadhi- Lugha ndicho chombo cha kuhifadhi na kueneza utamaduni
Matamshi na Lafudhi ya Kiswahili
Matamshini namna ambavyo mtu anatamka neno au jinsi mtu anavyozungumza lugha. Unaposema fulani ana matamshi mazuri ya Kiswahili utakuwa unamaanisha anazungumza Kiswahili fasaha.
Neno moja linaweza kuzungumzwa/kutamkwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali kutokana na sababu mbali mbali, sababu hizo ni pamoja na eneo la kijiografia anakotoka huyo mtu, kabila lake, kundi lake la kijamii mfano msanii au mwanasiasa, na elimu aliyonayo. Hizi zote zinaweza zikawa ni sababu za kufanya watu watofautiane katika matamshi.
Dhana ya matamshi huhusisha:
  • Sauti za lugha husika
  • Mkazo
  • Kiimbo.
Sauti za Lugha ya Kiswahili
Sauti za lugha ya Kiswahili hujumuisha irabu na konsonanti, ambazo kwa ujumla huunda sauti 24, irabu tano na konsonanti 19 (konsonanti x na q hazipo katika matamshi ya kiswahili). Sauti za Kiswahili hutamkwa kama zilivyoandikwa, kwa mfano maneno “data” au “dengue” wewe unayatamkaje? Wengi huyatamka kama yalivyo hata kama wakiwa wanazungumza kiingereza, hii ni kwa sababu maneno ya Kiswahili hutamkwa kama yalivyoandikwa.
Kwa hiyo unapotamka maneno ya Kiswahili ni sharti uzingatie sauti asilia za lugha ya Kiswahili. Kuna watu huwa wanaandika hivi “xaxa”, hii huwa unaitamkaje?Au “ucjal” huwa unaitamkaje? Kwa kufuata matamshi asilia ya Kiswahili “ucjal” itatamkwa “uchijal” sijui itakuwa ina maana gani sasa. Na pengine umekuwa ukitumia maandishi ya namna hii hata kwenye insha zako ukidhani upo sahihi au ni kwa mazoea tu, sasa kwa kuwa umejua matamshi sahihi ya Kiswahili ni yapi, utajifunza kuyatumia kwa usahihi katika maandishi rasmi na yasiyo rasmi.

Mkazo
Katika lugha ya Kiswahili kuna namna ya kutamka maneno ili kuleta maana mbali mbali, kwa mfano neno “barabara” litaleta maana husika kulingana na jinsi lilivyotamkwa. Hivyo, mkazo ni pale silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.
Kwa mfano:ba’bu, maya’i, rama’ni (mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba'ra (njia).Baadhi ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine. Kwa mfano: bara'bara (sawa sawa), Alha’misi

Kiimbo
Ni utaratibu maalum wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza katika utamkaji wa lugha fulani.
Katika utaratibu wa utamkaji, dhana ya Kiimbo huandamana pia na dhanna ya kidatu ( yaani , kiwango cha juu, cha chini au cha kati cha sauti katika usemaj), Kwa hivyo ni muhimu hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu. Wakati kiimbo kina maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha, kidatu kina maana ya kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati au kuwa chini.

Aina za viimbo
  • Kiimbo cha maelezo: Kiimbo cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida msemaji wa lugha akiwa kwenye kidatu chochote kile mawimbi sauti ya usemaji wake yanakuwa takriban katika mstari ulionyooka. Mfano, Mwalimu anafundisha.
  • Kiimbo cha maulizo: Kiimbo cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango tofauti vya kidatu kutegemeana na aina ya swali linaloulizwa. Mfano, mwalimu anafundisha?
  • Kiimbo cha amri: kiimbo cha amri hakitofautiani sana na kiimbo cha maulizo. Kiimbo cha amri, mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo katika kiimbo cha maelezo. Mfano, njoo hapa!
Lafudhi ya Kiswahili
Lafudhi ni matamshi ya msemaji wa lugha fulani ambayo yanatokana na athari za kimazingira. Mazingira hayo yanaweza kuwa eneo atokalo mtu, mahali alikosomea, kiwango chake cha elimu, tabaka lake la kijamii na kadhalika.
Lugha ya Kiswahili ni lugha ya pili kwa watumiaji wengi wa Afrika Mashariki, kwa hiyo hii inafanya kuwatambua wazungumzaji wa Kiswahili kulingana na makabila yao au maeneo wanakotoka. Kwa mfano, kwa hapa Tanzania tunaweza kuwatambua watu wa Mwanza kwa lafudhi yao, watu wa Mtwara kwa lafudhi yao, watu wa Pemba kwa lafudhi yao au watu wa Musoma kwa lafudhi yao. Mifano:
  1. Usiniretee maswara ya ubaguzi wa kikabira hapa (Wakuria)
  2. Amemupiga mutoto ya watu juu amemuibia mafaranga makumi mawili (Wakongo)
  3. Ukikaa nchale, ukichimama nchale (Wamakonde)
  4. Wewe unakamuaga mang’ombe tu moja kwa moja (Wasukuma)
  5. Mbona unakuwa kinganganizi, nilishakwambia sikupendi lakini wewe bado unaningangania tu! (Wahaya)







MADA YA PILI: AINA ZA MANENO
Katika lugha ya Kiswahili kuna angalau aina nane za maneno ambazo wataalamu wengi wa lugha wanakubaliana hivyo. Katika mada hii utaweza kujifunza na kubainisha aina zote nane za maneno na jinsi zinvyotumika katika sentensi. Utaweza pia kujifunza namna ya kutofautisha aina za maneno ambazo zimeleta ubishi miongoni mwa wataalamu wengi hususani katika Viunganishi na Vihusishi.

Ubainishaji wa aina Saba za Maneno
Aina Saba za Maneno ya Kiswahili
Bainisha aina saba za maneno ya Kiswahili
Aina za maneno katika lugha ya Kiswahili ni pamoja na hizi zifuatazo:
  1. Nomino (N)
  2. Viwakilishi (W)
  3. Vitenzi (T)
  4. Vivumishi (V)
  5. Vielezi (E)
  6. Viunganishi (U)
  7. Vihusishi (H)
  8. Vihisishi (I)
Ufafanuzi wa aina za Maneno
Nomino (N)
Nomino ni maneno yanayotaja vitu, watu, na hali kadhalika. Kuna aina mbali mbali za maneno ambazo ni pamoja na hizi zifuatazo:
  • Nomino za pekee:Nomino za pekee hutaja na kutambulisha nomino mahsusi na za kipekee. Yaani kuwa kitu ni hicho na wala si kingine chochote. Hizi ni nomino zinazohusisha majina kama vile ya watu, nchi, miji, mito, milima, maziwa na bahari. Herufi za kwanza za nomino za pekee huwa kubwa hata kama nomino hizi zinapatikana katikati ya sentensi.
  • Nomino za kawaida:Hizi kwa jina jingine huitwa nomino za jumla. Nomino hizi hazibainishi wazi wazi vitu ambavyo habari zake zinatolewa. Kwa mfano ikiwa ni mtu, mahsusi hatambuliwi. Haituambii kama ni Bahati, Bite ama Neema. Ikiwa ni mlima hautambuliwi kama ni Meru , Kilimanjaro au Evarest, yaani hutaja vitu bila kutaja umahususi wake kama ilivyo katika nomino za pekee.Hizi zinapoandikwa si lazima zianze na kwa herufi kubwa ispokuwa zimetumiwa mwanzoni mwa sentensi au zimetumika kama anuani ya kutajia kitu kama vile Mkuu wa Sheria. Katika mfano huu ‘sheria’ kwa kawaida ni nomino ya kawaida, lakini hapa inaanza kwa herufi kubwa kwani inataja anuwani ya kipekee.
  • Nomino za mguso:Nomino za mguso hurejelea vitu vinavyoweza kuhusika na mwanadamu kupitia milango ya hisia kama macho, mapua, masikio vidole na ulimi- yaani vitu vinavyoweza kushikika, kuonekana, kunusika na kuonjeka.
  • Nomino za jamii:Hizi ni nomino ambazo zinawakilisha vitu vingi katika jina moja, yaani nimino zinazotaja umla ya vitu vingi. Mfano; jozi ya viatu, umati wa watu, bustani ya maua, bunga ya wanyama
  • Nomiono dhahania:Kundi hili la nomino hutumia kigezo cha uwezekano wa kuhesabika kuziainisha. Hapa tunatofautisha kati ya nomino zinazowakilisha vitu vinavyohesabika kwa upande mmoja, na vile visivyohesabika kwa upande mwengine. Nomino ya vitu vinavyohesabikavitanda, nyumba,vikombe vitabu na kadhalika.Zile zisizohesabika hurejelea vitu ambavyo hutokea kwa wingi na haviwezi kugawika, kwa mfano maji, mate, makamasi, maziwa, moshi, mafuta. Aghalabu nomino hizo huwa sawa katika umoja na wingi.
  • Nomino za kitenzi jina:Hizi ni nomino zinazohusu vitenzi. Huundwa kwa kuongezwa kiambishi {ku-} cha unominishaji kwenye mzizi wa kitenzi cha kitendo halisi ili kukifanya kiwe nomino.
Vivumishi (V)
Vivimishi ni maneno yanayoelezea zaidi juu ya nomino, aghalabu vivumishi hutanguliwa na nomino. Kuna aina kadhaa za vivumushi, miongoni mwa hivyo ni pamoja na hivi vifuatavyo.
  • Vivumishi: vinaweza kujitokeza katika aina tatu ndogondogo.
  • Vivumishi vya sifa:hutoa sifa za nomino /kiwakilishi cha nomino. Sifa hizi huweza kuwa nzuri, mbaya au yoyote ile.
  • Vivumishi vya idadi;vivumishi vya aina hii hutoa taarifa kuhusu idadi ya nomino. Kuna vivumishi vya idadi vinavyoweza kuvumisha nomino kwa kutaja idadi ya nomino hizo kiujumla jumla bila kudhihirisha idadi halisi.
  • Vivumishi vya idadiambavyo huonyesha nafasi iliyochukuliwa na nomino fulani katika orodha.
  • Vivumishi vya kumiliki:-Ni vivumishi vinavyoonesha kuwa kitu fulani kina milikiwa na mtu au kitu kingine.
  • Vivumishi Vioneshi:vivumishi vya aina hii huonyesha mahali au upande kitu kilipo. Vivumishi vya aina hii hujengwa na mzizi{h}kwa vitu vilivyopo karibu na mzizi{le}kwa vitu vilivyo mbali.
  • Vivumishi vya kuuliza:Hivi ni vivumishi ambavyo hufafanua nomino kwa kuuliza habari zake. Hujibu swali “gani?ipi? ngapi?”
  • Vivumishi vya A- unganifu:Vivumishi vya aina hii huundwa kwa mzizi wa kihusishi a- unganifu. Kihusishi hiki huandamana na nomino kuunda kirai husishi ambacho huvumisha nomino iliyotajwa awali.Vivumishivya aina hii hutumika kuleta dhana za–Umilikaji, -Nafasi katika orodha.
  • Vivumishi vya jina kwa jina:Hizi ni nomino zinazotumika kama vivumishi ambazo hutumika kufafanua nomino
  • Vivumishi vya pekee:Vivumishi hivi huitwa vya pekee kwa sababu kila kimojawapo huwa na maana maalumu. Pia kila kimojawapo huchukua upatanisho wake wa kisarufi kulingana na ngeli ya nomino ambayo kinaivumisha.
Mizizi vivumishi hivi niote, o-ote, -enye, -enyewe, -ingine, -ingineo.
  • -ote:Huonyesha ujumla wa kitu au vitu
  • -o-ote:Kivumishi cha aina hii kina maana ya “kila”, “bila kubagua”
  • – enye:Kivumishi cha aina hii hutumika kuleta dhanna ya umilikishaji nomino fulani.
  • -enyewe:Kivumishi cha aina hii hutumika kuisisitiza nomino fulani.
  • – ingine:Kivumishi cha aina hii huonyesha/huonesha ‘tofauti na’ au ‘zaidi ya’ kitu fulani
  • – ingineo:Kivumishi cha aina hii hutumika kuonesha/kuonyesha ziadi.
Vielezi(E)
Vielezi ni maneno yanayofafanua vitenzi, vivumishi au vielezi vingine. Huweza kuarifu kitendo kilichotendeka kilitendeka wapi, namna gani na hata mara ngapi.
Aina za vielezi
Vielezi vya Mahali
Vielezi vya mahali hutoa habari kuhusu mahali ambapo kitendo kilifanyika. Aghalabu vielezi hivi huundwa kwa kutumia jina la mahali au kwa kuongeza kiungo -NI mwishoni mwa neno linaloashiria mahali.Kwa mfano:nyumbani, kazini, shuleni
Example 1
  • Mtoto huyo hajatulia nyumbani tangu alipotoka Mombasa.
  • Msipitie sokoni mkienda kanisani.
Vielezi vya wakati
Huelezea zaidi kuhusu wakati kitendo kinapofanyika; kwa mfano: jioni, jana, asubuhi, saa saba, mwaka juzi.
Example 2
  • Mzee Kasorogani amesema kwamba ataoga mwaka ujao
  • Musa alilazimishwa kuchimba mtaro saa sita usiku
  • Kisaka na Musa watakutana kesho
Vielezi vya Idadi
Vielezi vya idadi hutulezea kitendo kilifanyika mara ngapi.
Idadi Kamili:Vielezi vya Idadi Kamili hutaja idadi kamili ya mara ngapi kitendo kilifanyika. Kwa mfano:mara mbili, siku mbili kwa juma, mara kumi
Example 3
  • Gibi alimzaba kofi mara tatu na kisha akakimbia
  • Daktari alimwagiza mama huyo achukue dawa mara tatu kwa siku na arudi hospitalini siku mbili kwa mwezi
Idadi Isiyodhihirika:Vielezi vya Idadi Isiyodhirika huelezea kiasi ambacho kitendo kilifanyika bila kutaja kiasi kamili kwa mfano:chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani.
Example 4
  • Mwizi wa kuku alipigwa mara kadhaa kabla ya kuokolewa na polisi.
  • Yeye hunipigia simu mara kwa mara.
Vielezi vya namna au jinsi
Vielezivya namna hii huonyesha jinsi au namna kitendo kilivyotendeka.Vielezi vya namna vipo vya aina kadhaa.
Vielezi vya namna halisi
Hivi ni vielezi vinavyotumia maneno ambayo kimsingi yana sura ya vielezi moja kwa moja katika uainishaji wa aina za maneno.
Vielezi vya namna mfanano
Hivi ni vieleziambavyo hutumika kufananisha vitendo na vivumishi au nomino mbalimbali. Hujengwa kwa kuongeza kiambishi(ki-)au kiambishi(vi-).Viambishi hivi hujulikana kwa jina la viambishi vya mfanano. Mfano; Ulifanyavizurikumsaidia mwanangu.
Vielezi vya namna vikariri
Hivi nivielezi ambavyo hufafanua vitenzi kwa kurudiarudia neno moja mara mbili.
Vielezi vya namna hali
Hivi nivieleziambavyo hufafanua juu ya kitendo kilichotendeka kimetendeka katika hali gani.
Vielezi vya namna ala/kitumizi
Hivi nivielezi vinavyotaja vitu ambavyo hutumika kutendea kitendo
Vielezi vya namna viigizi
Hivi vinaelezea zaidi jinsi tendo lilivyofanyika kwa kuigiza au kufuatisha sauti inayojitokeza wakati tendo linapofanyika au kutokea.
Vielezi vya wakati
Vielezivya namna hii huonyesha wakati wa kutendeka kwa kitendo.Huweza kutokea kama maneno kamili au hodokezwa kwa kiambishi{po.}
Vitenzi
Kitenzi ni neno linaloeleza jambo lililotendwa au lililotendeka. Kitenzi huarifu lililofanyika au lililofanywa na kiumbe hai chochote kinachoweza kutenda jambo
Kitenzi cha Kiswahili huundwa na mzizi pamoja na viambishi vyenye uamilifu wa aina tofauti
Aina za vitenzi
  1. Vitenzi vikuu:Vitenzi vikuu ni vile ambavyo hubeba ujumbe muhimu wa kiarifu cha sentensi.
  2. Vitenzi visaidizi:Hivi hutoa taarifa ya kusaidia vitenzi vikuu. Hutoa taarifa kama vile uwezekano , wakati, hali n.k.Vitenzi visaidizi daima hutumika na vitenzi vikuu, ndivyo vinavyobeba viambishi vya wakati.
  3. Vitenzi vishirikishi: Hivi ni vitenzi vishirikishi ambavyo havichukui viambishi vya nafsi, njeo ama hali. Vitenzi vishirikishi vipungufu ni vya aina mbili, ambavyo ni kitenzi kishirikishi“ni” cha uyakinishina kitenzi shirikishi “si” si cha ukanushi.
  4. Vitenzi vishirikishi vikamilifu:Hivi huchukuwa viambishi viwakilishi vya nafsi, njeo na hata hali. Kwa mfano;ndiye, ndio, ndipo.
Kazi za kitenzi kikuu
  • Kueleza tendo linalofanywa na mtenda/mtendwa.
  • Kuonyesha wakati tendo linapotendeka
  • Kuonyesha hali ya tendo
  • Kuonyesha nafsi
  • Kuonyesha kauli mbali mbali za tendo
  • Kuonyesha urejeshi wa mtenda/mtendwa/ mtendewa/ kujitendea
Kazi za kitenzi kishirikishi
  • Kushirikisha vipashio vingine katika sentensi
  • Kuonyesha tabia fulani iliyopo au isiyokuwepo ya mtu fulani au kitu fullani.
  • Kuonyesha cheo au kazi anayofanya mtu.
  • Kuonyesha sifa za mtu.
  • Kuonyesha umoja wa vitu au watu
  • Kuonyesha mahali
  • Kuonyesha msisitizo
  • Kuonyesha umilikishi wa kitu chochote.
Aina za wakati katika kitenzi
  • Wakati uliopita
  • Wakati uliopo
  • Wakati ujao
Hali mbalimbali za kitenzi
  • Hali ya masharti
  • Hali ya kuendelea kwa tendo
  • Hali ya kutarajia, kuamuru na kuhimiza
Viwakilishi
Viwakilishi ni aina ya neno linaloweza kutumika badala ya jina/nomino .
Aina za viwakilishi
  1. Viwakilishi vioneshi au viwakilishi vya kuonesha:Viwakilishi vionyeshi hutumika badala ya nomino kwa kutumia kuonyesha nomino inayorejelewa bila kuitaja. Kwa mfano; huyu, yule, hapo, kule, humo. Huyu si mwenzetu kabisa; kule hakufai kwenda watoto.
  2. Viwakilishi vya nafsi: Kwa mfano:mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao
  3. Viwakilishi vya kuuliza/viwakilishi viuliziambavyo huashiriwa na mofu /kiambishi{-pi}ambavyo katika tungo hutanguliwa na kiambishi ngeli cha jina husika. Kwa mfano, Wangapi wameondoka? Kipi kimekosewa?
  4. Wiwakilishi vya urejeshiambavyo vinajengwa na shinaambapamoja na vipande vidogo vidogo –ye-, -o-, -cho-, vyo, lo, po, mo, kon.k ambavyo vinachaguliwa kulingana na ngeli ya majina yanayorejeshwa navyo. Mfano; aliyeondoko hatapewa chake.
  5. Viwakilishi vya idadi:Viwakilishi hivi hutuarifu kuhusu idadi ya nomino hiyo huweza kuwa kamili (halisi) au ya jumla.
  6. Viwakilishi vya pekee/vimilikishi:-Hivi ni aina ya vivumishi vya pekee kuwakilisha nomino. Hufuata sheria za upatanisho za nomino zinazowakilishwa. Mfano; '-angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao '. kwangu haingii megini, chako haikna thamani.
  7. Viwakilishi vya A-unganifu:- Viwakilishi hivi huundwa kwa kihusishi chaA-unganifukusimamia nomino iliyomilkiwa, inayochukuwa nafasi fulani katika orodha au nomino ya aina fulani. Kihusishi a-unganifu huandamana na nomino kuunda kirai husishi ambacho husimama mahali pa nomino. Mfano;ya kwakeyamemshinda,vya wazeehaviguswi.
  8. Viwakilishi vya sifa:Haya ni maneno ya sifa ambayo huchukua nafasi ya nomino katika setensi. Kwa mfano -eupe, -janja, -tamu
  9. Viwakilishi vya Idadi;Idadi Kamili- hutumia namba kuelezea idadi ya nomino. 'saba, mmoja, ishirini' -Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake. Idadi Isiyodhihirika- huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili: 'chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani'
Viunganishi
Ni maneno, kikundi cha maneno au kiambishi chenye kuunganisha maneno, kirai, kishazi au sentensi.Dhima ya kiunganishi ni kuunga vipashio viwili au zaidi vyenye hadhi sawa kisarufi.
Aina za viunganishi
  • Viunganishi huru:hivi ni viunganishi vinavyosimama pekee katika tungo, katikati ya vipashio vinavyoungwa.Viunganishi huru hujumuisha:
  • Viunganishi nyongeza/vya kuongeza, kama vile, na, pia, pamoja. Baba na mwanae wanacheza mpira, Alichukua chakula chote pamoja na akiba iliyokuwepo.
  • Viunganishi vya sababu/visababishi, mfano, kwa sababu, kwa kuwa, kwa vile, madhali, ili. Alimsogelea karibu ila ambusu, Atatumikia kifungo madhali amebainika kuwa na hatia.
  • Viunganishi vya uteuzi/chaguo. Mfano; au, Naweza kwenda nyumani au shuleni.
  • Viunganishi vya kutofautisha/vya kinyume:ila, lakini, kinyume na, japokuwa, ingawa, ilihali. Mfano; Mkumbatie lakini usimbusu.
  • Viunganishi vya wakati.Wakati mfano; Mwalimu aliuliza swali wakati yeye amesinzia.
  • Viunganishi vya masharti;ikiwa, iwapo, hadi. Mfano; utaruhusiwa kuingia hapa ikiwa umevaa mavazi yanaostahili.
  • Viunganishi vihusishi; miongoni mwa, kati ya; mfano: Jane alikuwa miongoni mwa washindi kumbi bora kitaifa.
  • Viunganishi tegemezi:ni viambishi ambavyo hutiwa katika kitenzi cha kishazi tegemezi ili kukiunga na kitenzi kikuu cha kishazi huru ambavyo kwa pamoja huunda sentensi changamano au shurtia. Mfano; -po-, -cho-, -o- Nili-po-amka…, Ali-cho-mwelez…, alizo-o-neshwa…n.k
Vihusishi
Ni maneno ambayo huonyesha uhusiano uliopo baina ya neno moja na jingine. Vihusishi aghlabu huonyesha uhusiano kati ya nomino au kirai nomino na maneno mengine.
Mambo yanayoweza kuonyeshwa na vihusishi
  • Huonyesha uhusiano wa kiwakati; Mfano, ni vizuri kupiga mswakibaada yachakula.
  • huonyesha uhusiano wa mahali: mfano, Ninaishikaribu nakwa Mtogole
  • huonyesha uhusiano wa kulinganisha: Amekulazaidi yauwezo wake.
  • huonyesha uhusiano wa umilikaji: Usiguse hicho kitabu nicha kwangu
  • huonyesha uhusiano wa sababu/kiini: nimerudi kwaajili yakuonana na mkuu wa shule.
Aina za vihusishi
  1. vihusishi vya wakati
  2. vihusishi vya mahali
  3. vihusishi vya vya kulinganisha
  4. vihusishi vya sababu
  5. vihusishi vya ala/kifaa mfano; -kwa
  6. vihusishi vimilikishi
  7. vihusishi vya namna; Kichwacha mviringo
  8. vihusishi ‘na’ cha mtenda mfano, amepigwana Juma.
Matumizi ya kihusishi “kwa”
  1. huonyesha mahali au upande: Mfano, amekwenda kwa mjomba wake.
  2. huonyesha sababu au kisababishi cha jambo: mfano; ninaishi kwa ajili yako.
  3. huonyesha wakati: mfano; sina nafasi kwa sasa.
  4. huonyesha sehemu fulani ya kitu kikubwa, mfano: Mpira umekwisha wakiwa wamefungana nne kwa tatu.
  5. huonyesha jinsi kitendo kilivyotendeka: Mfano; alimvuta kwa nguvu sana ndo maana limevunjika.
Vihisishi/Viingizi
Ni maneno ambayo hutumiwa kuwakilisha hisia fulani.
Vihusishi vinaweza kugawanywa katika makundi yafuatayo:
Vihisishi vinavyoonyesha mhemko au hisi kali
  1. vihisishi vya furaha
  2. vihisishi vya huzuni
  3. vihisishi vya mshituko
  4. vihisishi vya mshangao
Vihisishi vya maamrisho au msisitizo wa jambo au tukio
  1. vihisishi vya maadili
  2. vihisishi vya mwiitiko
  3. vihisishi vya ombi
  4. vihisishi vya bezo
  5. vihisishi vya kutakia heri
  6. vihisishi vya kukiri afya/jambo
  7. vihisishi vya kiapo
  8. vihisishi vya salamu
Matumizi ya aina za Maneno katika Tungo
Matumizi ya Aina za Maneno katika Tungo
Elezea matumizi ya aina za maneno katika tungo
Aina za maneno hutumika katika tungo kwa kutegemeana na lengo la msemaji. Kwa mfano kama lengo la msemaji ni kuonesha aina fulani ya hisia atatumia vihisishi katika tungo yake. Vilevile kama msemaji anahitaji kueleza kuhusu namna nomino inavyotenda, ilivyotendewa au inavyotendwa, atatumia kitenzi.

Matumizi ya Kamusi
Kamusi ni kitabu cha marejeo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani na kupangwa katika utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo wasomaji wanaweza kuelewa. Au kamusi ni orodha ya maneno yaliyo katika karatasi au nakala tepe yaliyopangwa kialfabeti na kutolewa maana pamoja na maelezo mengine na kuhifadhiwa katika kitabu, santuri, simu, tarakilishi au katika mfumo wowote wa kielekroniki.
Kamusi huweza kuwa ya lugha moja, yaani orodha ya maneno pamoja na maelezo yake yakiwa katika lugha moja

Example 5
Mfano:
chatu,ni nyoka mkubwa na mnene
Kamusi nyingine huwa za lugha mbili yaani orodha ya maneno ipo katika lugha moja na maelezo ya maana ya maneno hayo yapo katika lugha nyingine.

Example 6
chatu,npython
Kamusi ni hazina ya lugha inayohusika, kwani tofauti na vitabu vingine vya lugha, huwa na orodha ya maneno mbali mbali yanayotumiwa na wazungumzaji wa lugha ile pamoja na maana zake. Japokuwa wingi wa maneno hutegemea ukubwa wa kamusi, kitabu hiki kina manufaa makubwa kwa mtumiaji wake kwani humpatia msamiati asioufahamu pamoja na maana zake au humpatia maana zaidi ya maneno anayoyafahamu.
Taarifa zinazopatikana katika kamusi
Awali kamusi zilipoanza kutungwa zilikuwa ni orodha ya maneno magumu pamoja na maana zake. Kamusi za siku hizi huwa na taarifa zaidi ya maana. Miongoni mwa taarifa ambazo kamusi huwa nazo ni:
  • tahajia za maneno mfano. Tasinifu Vs Tasnifu, Burangeti Vs Blanketi, Kula Vs Kura, -ingine vs -engine
  • matamshi
  • sarufi ya lugha kama inavyojitokeza katika kila neno kama vile maumbo ya wingi wa nomino, vinyambuo vya neno kama vile chezesha, chezeka, chezea, mchezo, mchezajin.k ambavyo vinatokana na kitenzi cheza
  • maana
  • etimolojia ya neno (asili ya neno husika)
  • matumizi ya neno
Jinsi ya Kutumia Kamusi
Maneno yanayoingizwa katika kamusi hupangwa kwa utaratibu wa alfabeti. Maneno yanayoanza na herufi a, yote huwekwa chini ya herufi A. Maneno yanayoanza na herufi fulani nayo hupangwa katika utaratibu wa alfabeti kwa kuzingatia herufi ya pili, ya tatu, nne au tano ya neno kama mfano hapa chini unavyoonyesha.
Example 7
Mfano:ja, jabali, jabiri, jadhibika, jadi.
Maneno yote yanaanza na herufi [j]. herufi ya pili kwa maneno yote ni [a]. herufi ya tatu ni [b] na [d]. Kwa kuwa [b] hutangulia [d] katika mpangilio wa alfabeti maneno yenye [b] kabla ya yale yenye [d]. Kwa kuwa maneno yenye herufi [b] ni mawili itabidi tutazame herufi ya nne ya hya maneno ili tuchague litakaloorodheshwa mwanzo. Neno ‘jabali’ litaorodhewshwa kabla ya ‘jabiri’ kwa kuwa [a] (herufi ya nne) ya ‘jabali’ hutangulia [i] ya ‘jabiri’ ambayo pia ni herufi ya nne. Kisha tunatazama maneno yenye [d] kama herufi ya tatu. Hapa tunaangalia pia herufi ya nne ili kubaini neno litakaloandikwa mwanzo kati ya ‘jadhibika’ na ‘jadi’. Kwa kuwa [h] hutangulia [i] basi ‘jadhibika’ huorodheshwa mwanzo ndipo lifuatiwe na ‘jadi’.
Kwa hiyo hivi ndivyo unavyopaswa kutafuta neno kwenye kamusi. Nenda kwenye herufi ya neno unalotafuta alafu litafute kwa kufuata mlolongo huo huo wa herufi ya kwanza kuorodheshwa.
Neno linaloorodheshwa kwenye kamusi ili lifafanuliwe linaitwakidahizo.Kidahizo huandikiwa maelezo ya kukifafanua. Maelezo haya ni matamshi ya kidahizo, maana ya kidahizo, kategoria ya kisarufi, sentensi ya mfano wa matumizi ya kidahizo n.k. Kidahizo pamoja na maelezo yake ndio huitwakitomeo cha kamusi.

Example 8
Kitomeo cha kamusi
Dhabihu (kidahizo)nm(kategoria ya neno) mahali pa kuchinjia wanyama (maana ya neno).
Taarifa Ziingizwazo katika Kamusi
Fafanua taarifa ziingizwazo katika kamusi
Maana za maneno
Kwa mfano:Dhabihunm mahali pa kuchinjia wanyama.
Kategoria za maneno
Kategoria za maneno kama vile kielezi (ele), kitenzi (kt), kivumishi (kv), nomino (nm), kihisishi.
Mifano ya matumizi
Kwa mfano, Waiziraeli huwapeleka koondo wao kwenye dhabihu kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Lengo la kutoa mifano ni kumsaidia msomaji asiye fahamu vyema neno husika aelewe jinsi neno hilo linavyotumika.
Uingizaji wa nomino
Nomino nyingi katika lugha ya kiswaili zina maumbo ya umoja na wingi.
Mfano:dumenmma-
mkopo;nm mi-
Viambishi ambatishi huwekwa kando ya nomino kuashiria umbo la wingi la nomino.
Ngeli za nomino
Mfano:mkoponmmi- [u-/i-]
Kutafuta maana unayoitaka
Neno linaweza kuwa na maana moja au zaidi ya moja. Maana inapokuwa moja mtumiaji kamusi hana tatizo kwani hiyo ndiyo atakayoipata na kuichukua. Lakini neno linapokuwa na maana zaidi ya moja, mtumiaji kamusi hutatizika asijue ni ipi aichague. Ili kupata maana inayosadifu itafaa mtumiaji kamusi kutafuta maana ambayo inahusiana na muktadha wa neno linalotafutwa.
Mfano:kifungonm vi-
  1. kitu cha kufungia
  2. kitu kinachotumiwa kufungia vazi kama vile shati, gauni, suruali n.k
  3. adhabu ya mtu kuwekwa jela kwa muda fulani
Iwapo mtumiaji aliona neno ‘kifungo’ kwa muktadha wa: “Juma alihukumiwa kifungo cha miaka kumi baada ya kupatikana na hatia ya kubaka….” Maana ya mukatadha huu itakuwa ni ile maana ya 3 kwa sababu ndiyo yenye kuhusiana na muktadha ambapo neno kifungo limetumika na wala sio maana ya 1 wala ya 2.




















MADA YA TATU: FASIHI KWA UJUMLA
Dhima ya Fasihi
Dhana ya Fasihi
Fasihi; ni sanaa ya lugha inayoshughulikia masuala yanayomhusu binadamu matatizo yake, ndoto zake, matumaini yake, migogoro yake na jinsi anavyoingiliana na mazingira yake. (Wamitila, 2004).
Fasili hii imejaribu kufafanua vizuri kile ambacho fasihi inajihusisha nacho, kimsingi fasihi inajihusisha na wanadamu. Vitu vya msingi tunavyoviona katika fasili hii ni kwamba fasihi ni sanaa, na fasihi inatumia lugha lakini zaidi fasihi inajihusisha na wanadamu.

Dhima za Fasihi katika Jamii
Dhima za fasihi katika jamii ni pamoja na hizi zifuatazo:
  • Kuburudisha jamii:Pamoja na mambo mengine fasihi inalenga kuburudisha jamii. Kupitia takribani vipera vyake vyote, fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira, kwa mfano kupitia nyimbo, hadithi, mashairi na kadhalika.
  • Kuelimisha. Fasihi hutumika kama nyenzo ya kuelimisha jamii, kupitia fasihi wanajamii wanaweza kuelimishwa juu ya mambo mabalimbali, kama vile juu ya umuhimu wa kuishi kwa amani, umuhimu wa kijikomboa kifikra, umuhimu wa kujikomboa kiuchumi, ubaya wa ufisadi na kadhalika.
  • Kuonya jamii. Fasihi ina jukumu la kuhakikisha wanajamii wanakaa katika mstari wa maadili ya jamii husika. Kupitia fasihi wanajamii wanapewa mwongozo wa jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.
  • Kuunganisha jamii. Fasihi huleta watu katika jamii. Watu huunganishwa kupitia kazi mbalimbali za kifasihi, kwa mfano, kupitia nyimbo, miviga, vichekesho na kadhalika.
  • Kukuza lugha.Fasihi hutumia lugha kufikisha ujumbe wake katika jamii, lugha ya fasihi huwa ni ya kisanaa zaidi na hivyo kuifanya iwe yenye mvuto kwa wasikilizaji au wasomaji. Mtu anaposoma au kusikiliza kazi ya fasihi anapata ujuzi wa lugha. Lakini pia fasihi yenyewe inaweza kutumika kama chombo cha kukuza lugha. Wasimulizi na waandishi wa fasihi huhitaji kuwa na utajiri mkubwa wa lugha.
  • Kuhifadhi mila, tamaduni na itikadi za jamii. Kupitia fasihi simulizi, tamaduni na mila za jamii husika huhifadhiwa. Kwa mfano kupitia methali, misemo, nahau na vitendawili unaweza kujua mila na tamaduni za jamii husika.
  • Kukuza uwezo wa kufikiri. Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. Kwa mfano, vitendawili, ngano za mtanziko na kadhalika.
Aina za Fasihi
Kuna tanzu mbili za fasihi, ambazo ni fasihi andishi na fasihi simulizi.
Dhana ya Fasihi Simulizi
Fasihi Simulizi ni utanzu wa fasihi ambao unawakilisha sanaa ya lugha inayopitishwa kutoka kwa kizazi hadi kizazi kwa njia ya maneno/masimulizi ya mdomo.
Sifa na Dhima za Fasihi Simulizi
Sifa za Fasihi Simulizi
  • Hupitishwa kwa njia ya mdomo
  • Ufanisi wa sanaa katika fasihi simulizi hutegemea uwezo wa msimulizi, au wahusika.
  • Masimulizi yake yanaweza kuathiriwa na mazingira, hisia na hali
  • Ni mali ya jamii. Hakuna mtu fulani anayemiliki sanaa katika fasihi simulizi.
  • Inaweza kubadilika kutoka kizazi hadi kizazi, au mazingira mbalimbali kwa sababu hutegemea kumbukumbu ya msimulizi.
  • Aghalabu huwa na funzo fulan
Dhima za Fasihi Simulizi
  • Kuburudisha - Hufurahisha na kuchangamsha hadhira
  • Kunasihi- kutolea mawaidha na kuonyesha mwelekeo unaotarajiwa katika jamii.
  • Kuelimisha watu kuhusu vitu mbalimbali hasa mazingira yao
  • Kutambulisha jamii - jamii mbalimbali husifika kutokana na sanaa zao katika fasihi simulizi kama vile nyimbo.
  • Kuhifadhi na kudumisha utamaduni wa jamii
  • Kuunganisha watu - huleta watu pamoja
  • Kukuza lugha - fasihi huimarisha lugha kwa kuwa hutumia mbinu mbalimbali za lugha.
  • Kuliwaza - hutoa huzuni na kuleta matumaini.
  • Kupitisha muda - wakati mwingine fasihi simulizi hutumika kupitisha muda.
  • Fasihi simulizi ni chombo cha mawasiliano hususani kupitia ngomezi.
Dhana ya Fasihi Andishi
Fasihi Andishi ni aina ya sanaa ambayo hutumia maneno ya maandishi kupitisha ujumbe kwa hadhira.
Kuna tanzu kuu nne za Fasihi Andishi:
  1. Hadithi Fupi – Hii ni kazi ya fasihi andishi yenye kisa kimoja na mhusika mkuu mmoja na maudhui yake sio changamani.
  2. Riwaya –Ni kazi ya fasihi andishi yenye wahusika wengi na muundo changamani ni ndefu na maudhui yake ni mapana.
  3. Tamthilia- ni kazi ya kisanaa yenye muundo wa kiugizikaji inayowasilishwa katika maandishi.
  4. Mashairi - mashairi yakiwa yamechapishwa pia hutambulika kama fasihi andishi.
Sifa na Dhima za Fasihi Andishi
Sifa za Fasihi Andishi
  • Hupitishwa kwa njia ya maandishi
  • Ni mali ya mtu binafsi
  • Haiwezi kubadilishwa papo kwa papo
  • Hutumia mbinu za lugha na mbinu za sanaa katika uwasilishaji wake.

Dhima za Fasihi Andishi
  • Kukuza lugha
  • Kuhifadhi kazi ya sanaa katika maandishi
  • Kuburudisha
  • Kuelimisha
  • Kukashifu tabia zisizoandamana na maadili ya jamii
  • Kuonya, kuelekeza, kunasihi
Tofauti kati ya Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi
Zifuatazo ni tofauti kati ya Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi kama zilivyobainishwa katika jedwali hapa chini:

FASIHI SIMULIZI
FASIHI ANDISHI
1.
Huwasilishwa kwa njia ya mdomo na/au matendo.
Huwasilishwa kwa njia ya maandishi
2.
Ni mali ya jamii.
Kazi andishi ni mali ya mwandishi (na mchapishaji)
3.
Msimulizi anaweza kubadilisha sehemu Fulani
Kitabu kilichoandikwa hakiwezi kubadilishwa
4.
Huhifadhiwa akilini
Huhifadhiwa vitabuni
5.
Kazi simulizi hubadilika na wakati
Kazi andishi haibadiliki na wakati
6.
Huhitaji msimulizi na hadhira yake wawe mahali pamoja wakati wa masimulizi
Msomaji anaweza kusoma kitabu cha hadithi peke yake, mahali popote, wakati wowote
7.
Mtu yeyote anaweza kutunga na kusimulia
Ni lazima mwandishi na msomaji wawe na uwezo wa kusoma
8.
Hutumia wahusika changamano (wanyama, watu, mazimwi n.k)
Hutumia wahusika wanadamu.









MADA YA NNE: FASIHI SIMULIZI
Fasihi simulizi ni moja kati ya tanzu za fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Katika mada hii utajifunza na kisha utaweza kubainisha tanzu na vipera vya fasihi simulizi pamoja na ufafanuzi wake. Na pia utaweza kutofautisha kati ya kipera na kipera au kati ya utanzu na utanzu.

Ubainishaji wa Tanzu za Fasihi Simulizi
Tanzu za Fasihi Simulizi
Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili.
Tanzu za Fasihi Simulizi ni pamoja na hizi zifuatazo:
  1. Masimulizi/hadithi
  2. Semi
  3. Ushairi
  4. Mazungumzo
  5. Maigizo
  6. Ngomezi
Ufafanuzi wa Vipera vya Tanzu za Fasihi Simulizi
SIMULIZI/ HADITHI
Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulani. Ni masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na mtiririko wake huwa mwepesi au sahili. Urefu wa hadithi hutofautiana kutoka kitanzu/kipera kimoja hadi kingine. Kwa jumla zipo hadithi ambazo ni za kubuni na zingine za kihistoria. Baadhi ya vipera vya utanzu huu ni:
Ngano
Hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Vijipera vya kipera hiki ni:
  • Istiara – hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine iliyofichika. Yaani hadithi nzima ni kama sitiari.
  • Mbazi- hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au wa kumkanya mtu
  • Kisa- hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli.
Visakale
Masimulizi ya kimapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia. Kwa mfano hadithi za Liyongo
Mapisi
Maelezo ya historia bila kutia mambo ya kubuni.
Soga
Ni hadithi ndogo ndogo zinazohusisha utani na ucheshi kwa kiasi fulani. Hizi ni hadithi ambazo hutambwa katika mtiririko wa matukio ambao huzua kicheko. Soga hudhamiria kuchekesha na pia kukejeli.
Tarihi
Hizi ni hadithi ambazo husimulia au zimejengwa kwenye matukio ya kihistoria. Inawezekana matukio yanayosimuliwa yakawa ya kweli, yaani yalipata kutokea kihistoria.Hadithi hizi hutokea zaidi katika maandishi.
Visasili
Ni utanzu unaofungamana na imani za dini na mizungu ya jamii. Hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na mwenendo wake, kuhusu asili yao wenyewe, na maana na shabaha ya maisha yao. Mara nyingi hadithi hizi huaminiwa kuwa ni kweli tupu, na hutumika kuelezea au kuhalalisha baadhi ya mila na madhehebu ya jamii inayohusika.

Vipera vya Ushairi
Huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Katika utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani.
Nyimbo
Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Kipera hiki kimegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.
  • Tumbuizo:hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama vile ngomani au harusini. Bembea; hizi ni nyimbo za kubembeleza watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo hulenga kubembeleza watoto.
  • Kongozi:hizi ni nyimbo za kuaga mwaka.
  • Nyimbo za dini:hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu.
  • Wawe:hizi ni nyimbo za kilimo; huuimbwa wakati wa kulima.
  • Tenzi:hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha.
  • Tendi:hizi ni nyimbo ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa, wahusika wa tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa.
  • Mbolezi:hizi ni nyimbo za kilio au maombolezo.
  • Kimai:hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini.
  • Nyiso:hizi ni nyimbo za jandoni.
  • Nyimbo za vita:hizi ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita..
  • Nyimbo za watoto:hizi ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao.
  • Nyimbo za uwindaji:hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa shughuli au sherehe zao.
  • Nyimbo za Taifa:hizi ni nyimbo za kusifia Taifa au kabila.
  • Nyimbo za kazi:hizi ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima, kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi, useremala na kadhalika
Maghani
Maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa.
Kipera hiki kina vijipera vitatu ambavyo ni maghani ya kawaida,sifonamaghani masimulizi.
Maghani ya kawaidani kundi ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.
Sifo:hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli. Sifo huwa na tanzu muhimu kama vile vivugo (majigambo),pembezinatondozi.
  • Kivugo:hili ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe.
  • Tondozi:hizi ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu.
Ghani masimulizi:hizi ni ghani ambazo hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani. Ghani masimulizi ina vipera vinne ambavyo ni rara, ngano, sifo na tendi.
  • Rara ni hadithi fupi nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua; rara huimbwa au kughanwa ikiambatana na ala za muziki.
  • Ngano:hizi ni hadithi za mapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha.Ngano huwa ghani masimulizi inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.
  • Sifo:hizi ni tungo za kusifu: sifo huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika utondozi wake, lugha iliyotumika ni lugha ya kishairi.
  • Tendi:hizi ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito kijamii au kitaifa.
Vipera vya Semi
Semi ni tungo au kauli fupifupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo muhimu ya kijamii. Baadhi ya tanzu katika kundi hili ni:
  • Methali: Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa muhtasari fikra au mafunzo, mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Mara nyingi mawazo hayo huelezwa kwa kutumia tamathali hasa sitiari na mafumbo. Methali nyingi huwa na muundo wenye sehemu mbili. Sehemu ya kwanza huanzisha wazo fulani, na sehemu ya pili hulikanusha au kulikaamilsha wazo hilo. Kwa mfano; mwenda pole hajikwai, aliye juu mngoje chini.
  • Vitendawili: Ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili iufumbue. Fumbo hilo kwa kawaida huwa linafahamika katika jamii hiyo, na mara nyingi lina mafunzo muhimu kwa washiriki, mbali na kuwachemsha bongo zao. Vitendawili ni sanaa inayotegemea uwezo wa mtu kutambua, kuhusisha na kulinganisha vitu vya aina mbalimbali vilivyomo katika maumbile.
  • Misimu: Ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. Msimu ukipata mashiko ya kutosha katika jamii huweza hatimaye kuingia katika kundi la methali za jamii hiyo.
  • Mafumbo: Ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika. Fumbo hubuniwa na msemaji kwa shabaha na hadhira maalum, hivyo ni tofauti na methali au vitendawili ambavyo ni semi za kimapokeo.
  • Lakabu: Haya ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Majina haya huwa ni maneno au mafungu ya maneno yenye maana iliyofumbwa. Mara nyingi majina haya huwa ni sitiari. Baadhi ya majina haya humsifia mhusika, lakini mengine humkosoa au hata kumdhalilisha; Mifano: simba wa yuda- Hali Selassie, Baba wa taifa – Mwl Nyerere.
Vipera vya Maigizo
Maigizo ni mchezo ambao hutumia watendaji wa kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani kwa hadhira.

Uhakiki wa kazi za Fasihi Simulizi
Umuhimu wa Uhakiki wa Kazi za Fasihi Simulizi
Umuhimu wa uhakiki wa kazi za fasihi simulizi ni kubaini ubora wa kazi za fasihi simulizi, kubaini vipengele mbalimbali vya fani na maudhui, kupima namna kazi inavyoambatana na mazingira inamotokea, kupima kufaa na kutokufaa kwa fasihi simulizi, kubaini ukweli wa mambo yanayoelezwa, kuangalia uhalisi wa watu na mazingira katika jamii na kubaini umuhimu wa kazi ya fasihi katika jamii husika.

Vigezo vya Uhakiki wa Kazi za Fasihi Simulizi
Uhakiki wa kazi ya fasihi huzingatia vigezo viwili ambavyo vimegawanyika katika vipengele mbalimbali. Vigezo hivyo ni fani na maudhui. Katika kigezo cha fani mhakiki atazingatia muundo, mtindo, matumizi ya lugha, wahusika na mandhari wakati katika kigezo cha maudhui mhakiki atazingatia dhamira, migogoro, falsafa, msimamo na ujumbe.

Uhakiki wa Hadithi
Uhakiki wa hadithi kama ilivyo katika kazi nyingine za fasihi simulizi umejikita katika kuchunguza vipengele mbalimbali vya fani na maudhui. Vipengele vya fani ni muundo, mtindo, wahusika, mandhari na matumizi ya lugha. Aidha kwa upande wa maudhui, vipengele vyake ni dhamira, migogoro, falsafa, ujumbe na msimamo.

Matumizi ya Semi katika Hadithi
Uhakiki wa semi katika fasihi umejikita kuangalia usahihi wa matumizi ya vipengele mbalimbali vya lugha katika kazi ya fasihi inayohusika. Vipengele hivyo ni misemo, nahau na mafumbo. Vilevile uhakiki wa semi umejikita katika kuchunguza namna lugha ilivyofuzu kigezo cha kwenda na wakati.










MADA YA TANO: USIMULIZI

Usimulizi ni jumla ya maelezo yanayotolewa na mtu au watu wengi kuhusu tukio fulani. Katika mada hii utajifunza juu ya taratibu za usimulizi wa matukio kupitia njia kuu mbili za masimulizi, yaani kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi. Pia utaweza kujifunza juu ya mbinu mbalimbali za usimulizi.
Usimulizi wa Hadithi
Usimulizi hufanyika kwa njia kuu mbili yaani kwa njia ya maandishi na kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Kila njia hutegemea namna msimuliaji anavyoweza kuwasiliana na msikilizaji. Ikiwa msimuliaji na msikilizaji hawakukaribiana, njia ambayo itatumika ni ile ya maandishi. Kwa mfano kama utahitaji kumweleza mtu aliyembali kuhusu tukio fulani la kusisimua utalazimika kutumia maandishi, yaani utatumia njia ya kumwandikia barua.
Lakini kama unamsimulia mtu ambaye yupo karibu nawe, utatumia njia ya mazungumzo ya ana kwa ana.

Usimulizi wa Habari
Taratibu za Usimulizi wa Matukio
Usimulizi wa matukio dhamira yake ni kumweleza mtu au watu tukio ambalo wao hawakulishuhudia. Hivyo katika usimulizi msimuliaji hutakiwa kutoa maelezo muhimu ambayo yatawawezesha watu hao kulielewa tukio linalosimuliwa sawasawa na huyo anayeshuhudia.
Mambo muhimu ya kutaja katika usimulizi wa matukio ni pamoja na haya yafuatayo:
  1. Aina ya tukio – msimuliaji atatakiwa kubainisha katika maelezo yake aina ya tukio. Kwa mfano, kama ni harusi, ubatizo, ajali ya barabarani au mkutano.
  2. Mahali pa tukio – ili msimuliaji aweze kuielewa habari inayosimuliwa, ni lazima kumwelewesha ni mahali gani tukio hilo limetokea. Kwa mfano, kama ni mjini inafaa kutaja hata jina la mtaa.
  3. Wakati – katika usimulizi ni muhimu pia kutaja muda ambao tukio limetendeka kama ni asubuhi, mchana au jioni bila kusahau kutaja muda halisi yaani ilikuwa saa ngapi.
  4. Wahusika wa tukio – ni muhimu kutaja tukio limehusisha watu gani, wingi wao, jinsia yao, umri wao n.k.
  5. Chanzo cha tukio – kila tukio lina chanzo chake hivyo ni muhimu kutajwa katika usimulizi.
  6. Athari za tukio – athari za tukio nazo ni sharti zibainishwe. Kama ni ajali, je watu wangapi wameumia; wangapi wamepoteza maisha n.k.
  7. Hatima ya tukio – msimuliaji katika usimulizi wake ni lazima abainishe baada ya tukio kutokea na kushughulikiwa hatima yake ilikuwaje. Kwa mfano, kama tukio ni ajali ya barabarani hatima yake inaweza kuwa majeruhi kupelekwa hospitalini na dereva aliyehusika kukamatwa.
Kwa hiyo misingi hii ya usimulizi hufanya usimulizi wa tukio kuwa na sehemu kuu tatu:
  • Utangulizi – sehemu hii huwa na maelezo tu ya utangulizi ambayo hulenga kuvuta hisia na umakini wa msikilizaji au wasikilizaji. Kwa kawaida utangulizi wa tukio huwa ni maneno machache kiasi yasiyozidi aya moja.
  • Kiini – kiini cha usimulizi huelezea tukio halisi kuanzia chanzo chake, wahusika, muda, mahali na athari za tukio.
  • Mwisho – mwisho wa usimulizi ni matokeo yanayoonyesha matokeo ya mwisho ya tukio linalohusika, wakati mwingine matukio haya yanaweza kuambatana na maelezo ya msimuliaji kuhusu mtazamo au maoni yake binafsi juu ya tukio ambalo amesimulia.
Mbinu za usimulizi
Ili habari inayosimuliwa ipate kueleweka vizuri, sharti msimuliaji ajue mbinu za kusimulia katika hali inayovuta hisia za msikilizaji wake.
Baadhi ya mbinu hizo ni uigizi, utumizi wa lugha fasaha inayozingatia lafudhi sahihi ya Kiswahili.
Kwa upande wa uigizi msimuliaji atatakiwa kuigiza mambo muhimu yanayohusiana na tukio ambalo anasimulia. Nayo ni kama vile milio, sauti na matendo.
Kwa upande wa usimulizi ambao unafanyika kwa njia ya maandishi, sharti usimulizi huo uwe na kichwa cha habari. Kichwa cha habari kinatakiwa kuandikwa kwa maneno yasiyozidi matano, yaliyoandikwa kwa herufi kubwa.
Kwa vile usimulizi wa tukio huwa unahusu tukio lililopita, maelezo yake mengi huwa katika wakati uliopita.












MADA YA SITA: UANDISHI WA INSHA
Uandishi Wa Insha
Uandishi ni kitendo cha kupangilia maneno katika maandishi. Mada hii inazungumzia uandishi wa insha za wasifu kwa umahususi wake. Kabla ya kuanza uandishi utajifunza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika uandishi wa insha kwa ujumla. Utaelewa muundo wa insha na mwisho utajifunza juu ya dhana ya insha ya wasifu na namna inavyoandikwa na mwisho kabisa utaangalia mfano wa insha ya wasifu.

Insha za Wasifu
Insha ya wasifu ni ile ya kutoa maelezo juu ya jinsi mtu au kitu kilivyo, tabia, vitendo na mandhari (sura ya mahali jinsi panavyoonekana).
Mambo muhimu katika insha ya wasifu ni: sura, rangi, umbo, vipimo, tabia, na kadhalika. Insha hizi zinaweza kuongelea kitu chochote kile, inaweza kuwa ni mnyama, mtu, Shule, nchi na kadhalika.

Hatua za Uandishi wa Insha
Kabla ya kuanza kuandika insha, ni muhimu sana uamue unataka kuandika juu ya nini. Inafaa uchague ile mada iliyo rahisi kwako kuweza kujieleza kikamilifu na kwa urahisi.
Kama unaandika insha za kufanyia mazoezi ni heri uchague mada zenye habari ambazo unazielewa. Iwapo hulijui au hulielewi jambo, ufanye uchunguzi kwanza. Ukisha kupata habari muhimu ndipo baadaye uandike insha yako kulingana na jinsi unavyoijua na jinsi unavyoikumbuka habari inayohusika.
Katika mtihani ni muhimu uyasome maagizo kwa makini. Kwa mfano, maagizo yanaweza kuwa: Chagua mojawapo ya habari zifuatazo kisha uandike insha isiyopungua kurasa mbili za karatasi za majibu.
Au:
Chagua mojawapo ya habari hizi kisha uandike insha ya maneno yasiyopungua 400.
Ni heri uandike insha nzuri ya kiwango kinachotakiwa kuliko ndefu (zaidi ya maneno 400) ambayo haitakuwa na mambo muhimu hadi mwisho, na pengine yenye makosa na uchafu mwingi kupindukia. Ni muhimu ikumbukwe jinsi insha ilivyo ndefu, hasa katika mtihani, ndivyo idadi ya makosa inavyozidi kuongezeka.

Muundo wa Insha
Katika uandishi wa insha, muundo wake unakuwa na vitu vifuatavyo:
  1. Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya n.k
  2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako.
  3. Kiini cha insha; katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.
  4. Hitimisho; hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichohadiliwa katika insha.
Hebu soma mfano ufuatao wa insha ya wasifu:
Mfano 1
SHULE YANGU
Shule yangu inaitwa Shule ya Sekondari ya Mwananchi. Ni shule ya zamani iliyoanzishwa siku ya Ijumaa, tarehe 5 Agosti 1966 na Mheshimiwa Donna Matembele, aliyekuwa diwani wa kata ya Masuba.
Shule hii ambayo ni maarufu sana ipo katika Tarafa ya Mkunazini. Imejengwa katika uwanja wa hekta kumi na mbili. Ina madarasa kumi na mawili ya vidato vinne vya mikondo mitatu kila kimoja. Ina wanafunzi mia tano na wanne badala ya idadi halali ya wanafunzi mia nne themanini. Ni shule inayopendwa sana.
Wanafunzi wa kike ni mia mbili na watatu na wa kiume ni mia tatu na mmoja. Walimu ni thelathini na mmoja. Jamii hii inapendana sana. Wanafunzi wana imani kubwa sana na walimu wao. Walimu huwahimiza wawe wanafanya bidii katika kazi na masomo kwa ujumla.
Wanafunzi hukadiria ugumu wa mazoezi wapewayo. Yale wayaonayo kuwa ni rahisi wao hujifanyia. Yale magumu kidogo hushughulikia kwa pamoja kwa kusaidiana wenyewe kwa wenyewe. Walimu hushirikishwa tu wakati wa mazoezi tata.
Shule ya Sekondari ya Mwananchi ni ya kuvutia sana. Ina miti mingi sana ya matunda. Ina maua ya aina aina. Kutokana na nidhamu na uwajibikaji matunda hukomaa ndipo yatumiwe kwa mpango wakati wa chakula.
Heshima imethaminiwa mno na wanafunzi. Wanaheshimiana na kuwaheshimu walimu wao. Kwao heshima ni utiifu na uzingativu. Kutii na kuzingatia mambo waambiwayo na walimu ndicho kipimo cha heshima.
Katika shule yangu wanafunzi tuko kama paka. Paka hamtumi mtu nyama lakini atunukiwapo kipande hawezi kumruhusu yeyote kukigusa.Nasi tutunukiwapo nafasi yoyote ya kusoma hatumruhusu mtu yeyote kutupokonya nafasi hiyo.
Wanafunzi wa shule wana sare zao za kuvutia wazivaazo kiungwana kabisa. Sare hizo ni sweta ya bluu, shati au blauzi ya samawati, tai ya rangi ya damu ya mzee, suruali ndefu au sketi ya kijani kibichi, viatu vyeusi vya soli ndogo na visigino vifupi.
Katika shule yetu kuna uhusianao mwema baina ya walimu, wazazi, Chama cha Wazazi na Walimu (CHAWAWA) na Baraza la Shule. Kamati ya CHAWAWA na Baraza la Shule huanzisha miradi na kuitekeleza haraka kutokana na wazazi kuiunga mkono.
Kwa muda mrefu sasa matokeo ya mitihani yamekuwa ya kuridhisha kabisa.Na si hayo peke yake. Wanafunzi washirikipo katika michezo ya mpira, ya riadha na matamasha ya muziki takribani mara zote huibuka washindi.
Kwa ufupi shule yangu ni ya mafanikio mengi.
Mambo muhimu ya kuzingtiwa katika insha hii ya wasifu:
  • KICHWA (Shule yangu).
  • MAELEZO KAMILI yenye:
  • JINA la shule
  • HISTORIA ya shule
  • MAZINGIRA ya shule
  • IDADI ya wanafunzi na walimu
  • HALI ya wanafunzi
  • MAFANIKIO ya shule.
  • HITIMISHO lenye sifa ya jumla.
Insha za Kisanaa na zisizo za Kisanaa
Tofautisha insha za kisanaa na zisizo za kisanaa
Zoezi 1
Tofautisha insha za kisanaa na zisizo za kisanaa

















MADA YA SABA: UANDISHI WA BARUA
Uandishi Wa Barua
Barua za kirafiki ambazo pia huitwa za kidugu huandikwa baina ya watu wa undugu au jamii moja. Katika mada hii utaweza kujifunza muundo wa uandishi wa barua ya kirafiki na jinsi ya kuandika barua ya kirafiki. Utaweza kutofautisha kati ya barua ya kirafiki na ile isiyokuwa ya kirafiki.

Barua za Kirafiki
Iwapo ni katika ndugu barua za kirafiki zaweza kuwa kwa watu kama: baba, mama, shangazi, mume, mke, mtoto, na kadhalika. Katika jamii waandikiwao barua za kirafiki ni kama jirani, rafiki, mpenzi, mwalimu, mwanafunzi, daktari, mgonjwa, na kadhalika.

Muundo wa Barua za Kirafiki
Mambo muhimu ya kuzingatia katika uandishi wa barua za kirafiki:
  • ANWANI kamili ya mwandishi, katika herufi hukaa juu upande wa kulia mwa karatasi.
  • TAREHE, chini ya anwani.
  • MTAJO wa heshima kwa anayeandikiwa, kama vile, mpendwa, mpenzi, na kadhalika, huandikwa kushoto, baada ya tarehe.
  • UTANGULIZI wa barua yenyewe ambao kwa desturi huwa ni salamu.
  • BARUA YENYEWE ambayo ndiyo kiini cha waraka.
  • SALAMU za kumalizia, pengine kwa jamaa na jamii.
  • HITIMISHO, katika aya, maalumu ambayo huwa, kwa mfano: ‘Ni mimi baba yako akupendaye,’ na kadhalika.
  • SAHIHI ambayo si sharti wala muhimu sana.
  • JINA au MAJINA ya mwandishi, mwishoni.
Tazama mfano wa barua ya kirafiki:

Mfano 1
MUSOMA FISH PACK
S.L.P 4546
MUSOMA
23/5/2013
Mwanangu Nyamchele,
Ninafuraha kukujulisha kuwa nimepokea barua yako. Mambo yote uliyoyaeleza nimeyaelewa barabara. Huku nyumbani sote tu wazima na ni matumaini yetu kwamba afya yako ni nzuri.
Tabia ya kulalamikia chakula ni mbaya. Tabia kama hii ikikomaa husababisha ulafi. Kumbuka hukwenda shuleni kula kama nguruwe. Huko shuleni nimekupeleka ili usome kwa bidii na ujifunze mengi. Usitamani kustarehe na kufikiria maakuli na anasa zingine za ulimwengu huu. Ondoa fikira za chakula akilini mwako na uache uzembe, eboo!
Hebu nikuonye kuhusu kuwapima na kuwachagua walimu. Walimu katika shule hiyo ni wabobezi na ndio maana nikakupeleka hapo. Wanajua mnayostahili kufundishwa. Huna ruhusa ya kusema eti walimu wengine ni wakali na hufundisha haraka haraka sana. Wewe unahitaji kutega sikio na kutii. Ukiwa makini na uwe na imani utayaelewa mambo unayofundishwa. Usisahau kuwa mchagua jembe si mkulima.
Mambo makubwa unayostahili kuyatilia bidii ni masomo yako. Muda wa miaka minne ni mfupi sana. Uonyeshe adabu njema kila wakati. Uwaonyeshe walimu wako taadhima na uwatii daima dawamu.
Jambo lililo kubwa katika shughuli yoyote ni uvumilivu. Ukivumilia utavuna matunda mabivu.Sitachoka kukusisitizia, ‘Ukilima pantosha, utavuna pankwisha.’ Fanya kila jitihada utimize mambo mengi iwezekanavyo kuanzia leo lakini usipapie chochote. Ndo ndo ndo hujaza ndoo.
Mungu akubariki.Umwombe akusaidie katika kila jambo. Ujiepushe na maovu yoyote yale. Ukiwa na jambo usiwe na hofu kutuarifu mara moja. Mama yako amekusalimu sana. Amenikumbusha nikupashe hakuna refu lisilo na ncha.
Kwaheri kwa sasa.
Ni mimi, baba yako akupendaye,
Magafu Malima












MADA YA NANE: UFAHAMU
Ufahamu ni dhana inayorejelea kujua na kulielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea upya kwa usahihi bila kupoteza maana yake ya msingi. Ufahamu wa mtu waweza kupimwa katika kusikiliza jambo au katika kusoma.

Kusikiliza
Ufahamu wa kusikiliza ni zaidi ya kusikiliza tu kile kilichosemwa; badala yake ni uwezo wa mtu kuelewa maana ya maneno anayoyasikia na kuweza kuhusiana nayo kwa namna fulani. Kwa mfano mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake mwenyewe.
Mambo ya Kuzingatia katika Ufahamu wa Kusikiliza
Elezea mambo ya kuzingatia katika ufahamu wa kusikiliza
Ufahamu wa kusikiliza unahusisha michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa. Michakato hii inahusisha:
  • Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa
  • Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza
  • Kuelewa sintaksia (muundo wa maneno) ya sentensi kwa namna zinavyowasilishwa.
Katika ufahamu wa kusikiliza, msikilizaji hana budi kuzingatia mambo yafutayo:
  1. Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili kuweza kusikia kila anachokisema.
  2. Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo msemaji anaongeza jambo jipya, anatofautisha, anafafanua au anahitimisha hoja.
  3. Msomaji anatakiwa kuandika baadhi ya mambo anayoona kuwa ni ya muhimu ili kumasidia kukumbuka hapo baadae.
  4. Kuwa makini na ishara mbambali za mwili kama vile kurusha mikono, kutingisha kichwa, kutingisha mabega au hata kupepesa macho. Ishara hizi huwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kupata maana katika mazungumzo.
Kujibu Maswali kutokana na Habari uliyosikiliza
Jibu maswali kutokana na habari uliyosikiliza

Zoezi 1
Jibu maswali kutokana na habari uliyosikiliza

Kusoma kwa Sauti
Kusoma kwa sauti ni namna ya kuyaangalia maandishi na kuyatamka kwa sauti inayosikika.
Mambo ya Kuzingatia katika Ufahamu wa Kusoma
Elezea mambo ya Kuzingatia katika ufahamu wa kusoma kwa sauti
Kuna vipengele viwili vinavyounda mchakato wa ufahamu wa kusoma:
  • Uelewa wa msamiati na
  • Uelewa wa matini
Ili kuilelewa habari/matini ni lazima msomaji awe na uwezo wa kuelewa msamiati uliotumika katika matini hiyo. Endapo maneno yaliyotumika hayataeleweka vilevile matini yote haitaeleweka.
Katika ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
  1. Kubaini mawazo makuu; msomaji anaposoma habari fulani au kitabu inatakiwa ajiulize, Je, kinachoongelewa hapa ni nini? Ni jambo gani hasa analolizungumzia mwandishi? Msomaji akiwa na maswali haya akilini mwake basi itakuwa rahisi kwake kuielewa habari hiyo.
  2. Kuzingatia alama za uakifishi; msomaji ni lazima azingatie alama za uakifishi, kwa kufanya hivyo itamsaidia kuelewa ujumbe wa habari hiyo na endapo hatazingatia alama za uakifishaji anaweza kupotosha maana ya mwandishi.
  3. Kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali; habari nyingine huwa zina maneno ya kisanaa hivyo ni muhimu msomaji kubaini maana ya maneno hayo katika muktadha wa habari hiyo, hii itamsaidia kuelewa vyema maana ya mwandishi.
  4. Vilevile msomaji anatakiwa kumakinikia kile anachokisoma, kila kipengele anachokisoma inampasa akielewe vizuri.
Kwa kuzingatia haya yote msomaji atakuwa na uelewa mzuri juu ya habari aliyoisoma na pia anaweza kufupisha habari hiyo aliyoisoma.
Kujibu Maswali kutokana na Habari uliyosoma
Jibu maswali kutokana na habari uliyosoma
Zoezi 2
Jibu maswali kutokana na habari uliyosoma

Kusoma Kimya
Kujibu Maswali kutokana na Habari uliyoisoma
Katika usomaji huu, msomaji hufumba kinywa na kupitisha macho katika kila mstari harakaharaka. Macho hayo huunganisha neno lililotangulia na lile linalofuata. Ubongo wake huchambua mambo muimu yanayojitokeza, huku akiyahifadhi kichwani. Mtu akijizoeza kusoma kimya, ananufaika ifuatavyo:
  1. Hupata nafasi ya kupima mwendo wake na kiasi cha welewa
  2. Hujiepusha na lawama ya kusumbua wengine
  3. Hukwepa kuzingatia kanuni za matamshi
  4. Huweza kusoma maandishi mengi kuliko ambavyo angesoma kwa sauti
Kusoma kwa Burudani
Huu ni usomaji ambao lengo lake kuu huwa ni kujiburudisha tu. Katika usomaji wa aina hii, msomaji hujisomea zaidi magazeti, majarida na vitabu tofauti na vile vinavyotumika darasani.
Mambo ya Kuzingatiwa katika Ufahamu wa Kusoma kwa Burudani
Fafanua mambo ya kuzingatiwa katika ufahamu wa kusoma kwa burudani
Wakati mwingine sio lazima msomaji awe na vitabu vyote ambavyo anahitaji kuvisoma au magazeti na majarida. Inapotokea hivyo, msomaji anaweza kwenda maktaba kuazima kitabu nachokihitaji.
Ingawa lengo la msomaji huwa ni kujiburudisha tu, lakini pia hujiongezea maarifa. Hii ni kwa sababu, magazeti, majarida na vitabu sambamba na kutuamia lugha sanifu huelezea mambo mabalimbali yanayoihusu jamii.
Hivyo msomaji kutokana na kusoma vitabu na majarida mbalimbali hujiongezea kiwango cha welewa wa lugha na mambo mengine ya kijamii yanayojadiliwa humo.
Ni jambo zuri kwa msomaji kujijengea tabia ya kujipima ili aweze kuelewa kiwango cha maarifa aliyopata katika kujisomea. Kujipima huku kunaweza kufanywa kwa kujiundia utaratibu wa kuweka kumbukumbu ya vitu au makala zilizosomwa na kufanya ufupisho wa kila makala.
Utaratibu unaopendekezwa katika kujipima na kujiwekea kumbukumbu ya usomaji wa burudani ni kama ufuatao:
  1. Tarehe...
  2. Jina la kitabu/makala/gazeti....
  3. Mchapishaji......
  4. Mwaka/tarehe ya uchapishaji.....
  5. Ufupisho wa habari(yasizidi maneno 20)
  6. Fundisho/ujumbe mkuu ni.....
  7. Jambo lililokuvutia sana......
  8. Maoni kwa ujumla kama yapo....


Ndugu mwalimu/mwanafunzi kama unapata changamoto yoyote ile 
kuhusu upatikanaji wa NOTES HIZI kwenye website hii, tafadhari wasiliana nasi kwa 
simu no/hotline. 0759-104804 Paschal kabonge
barua pepe. paschalkabonge2@gmail.com
au andika maoni yako kwenye sehemu ya comment hapa chini ya post hii.
Kumbuka: mitihani yote inapatikana bureeee kabisa.
Asante.
ELIMU NI HAKI KWA WOTE.

Post a Comment

0 Comments